HAWA NDIO MBWA WENYE AKILI ZAIDI DUNIANI


Na Daniel Mbega,MaendeleoVijijini Blog

WANYAMA wa wa kufugwa wao wa aina nyingi sana. Wapo ambao wanafugwa kwa ajili ya kitoweo, wapo wanaofugwa kwa mapambo, wapo tunaowafuga kama wanyama-kazi, na wapo pia wa mapambo ambao tunawatumia pia kwa ulinzi.

Ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, sungura, simbilisi au sili, kuku na jamii zote za ndege, hawa tunawafuga kwa ajili ya kitoweo.

Maendeleo Vijijini inatambua kwamba, wanyama wanaofugwa kwa ajili ya wanyama-kazi ni punda na farasi, lakini pia ng’ombe anatumika kama mnyama kazi kwa kuvuta mikokoteni na kulima kwa kutumia plau pezi, wakati ambapo farasi anaweza kutumika kwa usafiri huku punda akitumika kubeba mizigo na hata kuvuta mikokoteni.

Paka anafugwa kwa ajili ya mapambo, lakini ni mlinzi pia kwa sababu anapambana na wanyama wadogo waharibifu, hususan panya.

Sungura nao wapo wanaofugwa kwa mapambo na wapo wanaofugwa kwa nyama na mambo mengine.

Mbwa ndiye mnyama ambaye kwa asilimia kubwa anafugwa kwa ajili ya ulinzi, japo mara chache hufugwa kwa mapambao kutegemeana na aina ya mbwa mwenyewe.

MaendeleoVijijini leo inazungumzia kuhusu aina mbalimbali za mbwa, hususan wenye uwezo mkubwa na akili kuliko jamii nyingine.

Unaweza kushangaa, lakini wanyama hawa ni werevu na aina zifuatazo zinawaelezea kwa kina zaidi;

1 - BORDER COLLIE

Mbwa jamii ya Border Collie walianza kufugwa kwa nia ya kukusanya na kuchunga kondoo katika eneo la milima la mpaka wa Scotland na England. Mbwa hawa wanafahamika kutokana na mtazamo wao, yaani macho, ambao huutumia kulinda kundi la kondoo.

Kondoo wenyewe wakiwaona tu wanatulia kwa namna wanavyowatazama.

Mbwa hawa wana nguvu nyingi, stamina, na wana bidii ya kazi, mambo yanayomfanya awe mbwa bora zaidi kwa ajili ya kuchunga, na ndiyo maana anaitwa mbwa mchungaji; mpaka sasa bado anatumiwa kuchunga kondoo katika mashamba makubwa na ranchi za wanyama ulimwenguni.

Maendeleo Vijijini inatambua kwamba, mbwa wa jamii ya Border Collie aliyefunzwa kwa kiwango kikubwa na mwenye akili pia anaweza kushiriki katika mashindano na michezo ya wanyama, kama utiifu, kuruka, kukimbi, kukimbiza mpira na mashindano mengine kama hayo.

Kwa ujumla, mbwa jamii ya Border Collies wana maumbo ya kati na ngozi ya rangi mbalimbali, japokuwa rangi nyeupe na nyeusi ndiyo maarufu. Mbwa dume wa jamii hii ana urefu wa kati ye sentimeta 48 hadi 56 wakati jike ana urefu wa kati ya sentimeta 46 na 53.

Mbwa wa jamii ya Border Collies ndio wanaotajwa kuwa na akili kuliko wote duniani na imekuwa ni jamii maarufu kama mbwa wa mapambo kutokana na kufundishika kufanya mambo mbalimbali.

Mbwa hawa wanaweza kuishi kati ya miaka 10 na 14, ingawa wastani wao ni miaka 12. Chanzo kikuu cha vifo vyao ni saratani (23.6%), umri mkubwa (17.9%) na matatizo ya ubongo (9.4%).

2 – POODLE

 

Mbwa wa jamii ya Poodle wako kundi la mbwa wa kawaida na wamegawanyika katika makundi matatu au manne ambayo niStandard Poodle, Medium Poodle,Miniature Poodle na Toy Poodle. Wanapatikana katika rangi mbalimbali.

Maendeleo Vijijini inajua kwamba, mbwa hawa wanashika nafasi ya pili kwa kuwa na akili nyingi nyuma ya Border Collie, lakini jamii hii wana uwezo mkubwa wa kushiriki michezo mingi ya wanyama pamoja na shughuli mbalimbali, wana

Toy Poodles walishinda mashindano ya "Best in Show" mwaka 1966 na 1982. Standard Poodles walishinda katika miaka ya 1955, 1985, 2002 na 2014.

Asili ya mbwa hawa inatatiza ingawa inaelezwa kwamba ni Ujerumani ambako walikuwa wakijulikana kama Pudelhund. Neno Pudel linatokana na lugha ya Kijerumani likimaanisha ‘kumwaga’, na neno Hund (maana yake mbwa). Wengine wanasema asili yake ni Ufaransa kutokana na mbwa aina ya Brbet ambaye inawezekana alipandishwa na jamii ya mbwa kutoka Hungary. Huko Ufaransa wanafahamika kama retriever kutokana na kutumiwa kutafuta vitu majini na wanajua kuogelea.

Mbwa wakubwa, yaani Standard Poodle, ni wawindaji wakubwa na wanaweza kuwinda hata ndege, wanaweza kuruka kwenye mashina ya miti na kadhalika. Wana akili sana kiasi kwamba wanapoelekezwa wanaelewa mara moja.

Katika maandiko na tafiti mbalimbali ambazoMaendeleoVijijini inazo, mbwa wa jamii hii waliwahi kutumiwa hata kwenye vita kuanzia karne ya 17, na wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia walitumika pia hasa kwenye majeshi ya majini.

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita huko Amerika ya Kaskazini, mbwa wa jamii ya Standard Poodle wamerejeshwa kwenye kazi yao ya mwanzo kabisa kama wawindaji wa bata na ndege.

Umri wa kuishi wa mbwa hao ni kati ya miaka 11.5 hadi 12. Vyanzo vikuu vya vifo vyao ni saratani (30%), uzee (18%), GDV (6%), na magonjwa ya moyo (5%).

3 - GERMAN SHEPHERD / ALSATION

 

 

 

 

 

 Mbwa wa jamii ya German Shepherd (Kijerumani: Deutscher Schäferhund) ni jamii ya mbwa wa maumbile ya kati na makubwa wanaofanya kazi ambao asili yao ni Ujerumani.

Awali huko Uingereza walijulikana kama Alsatian. Tangu ilipoendelezwa mwaka 1899, jamii ya Mbwa Mchungaji wa Kijerumani - German Shepherd – walikuwa wakitumika kuchunga kondoo.

Tangu wakati huo, kutokana na nguvu zao, akili, uwezo wa kufundishika, na utii, mbwa hawa wanapendwa ulimwenguni kote kwa ajili ya kazi mbalimbali, ikiwemo kuwasaidia walemavu, kutafuta na kuokoa, polisi na majeshi pia yanawatumia sana. Ndio wanaotumiwa hata kukamata dawa za kulevya, mabomu na kadhalika.

Mbwa Wachungaji wa Kijerumani wana maumbo ya kati na makubwa. Kimo chao ni kati ya sentimeta 60 – 65 kwa madume na sentimeta 55-60 kwa majike wakati uzito wao ni kati ya kilogram 30 – 40 kwa madume na kilogram 22 – 32 kwa majike.

4 - GOLDEN RETRIEVER

 Golden Retriever mi jamii ya mbwa wakubwa wanaofugwa kama mbwa wa bunduki – gun dogs – kwa ajili ya kutafuta na kukamata mabata maji na ndege wakati wa uwindaji, na waliitwa watafutaji kwa sababu ya uwezo wao wa kuwakamata ndege bila kuwadhuru na kuwapeleka kwa wahusika.

Mbwa hawa wanapenda sana kuogelea majini na ni rahisi kuwafundisha misingi na mbinu za hali ya juu.

Mbwa hawa ambao wanajiamini sana, wana uwezo wa kuishi kati ya miaka 11 na 12.

Asili ya mbwa hawa ni Scotland katikati ya karne ya 19. Wakati huo uwindaji wa kanga ulikuwa mchezo maarufu kwa matajiri wa Uskochi.

5 - DOBERMAN PINSCHER

 Mbwa jamii ya Doberman Pinscher wana maumbile makubwa ya kati na walianza kufugwa mwaka 1890 na Karl Friedrich Louis Dobermann, mtoza ushuru wa Ujerumani. Meno yake ni marefu na kama watang’ata basi wanaleta madhara makubwa.

Mbwa wa kawaida wa jamii hii ana urefu wa kati ya sentimeta 69 hadi 72. Dume mara nyingi huwa na uzito wa kilogram 40 hadi 45 na jike kilogram 32 hadi 35.

6 - SHETLAND SHEEPDOG


Shetland Sheepdog, au Sheltie, kama jina lao lilivyo, ni mbwa wachungaji. Jina la asili la mbwa hawa ni Shetland Collie, lakini hili likaleta mkanganyiko miongoni mwa wafugaji wa mbwa jamii ya Collie wakati huo, hivyo jamii hii ikaitwa Shetland Sheepdog.

Kulingana na tafiti mbalimbali ambazo MaendeleoVijijini inazo, mbwa hawa wadogo kwa maumbile wana akili, wanabweka sana, wanafurahishhah, wana nguvu na wanafanya kazi kwa nguvu. Jamii hii ilitambuliwa rasmi la klabu maarufu ya jamii za mbwa ya The Kennel Club mnamo mwaka 1909.

Historia yake ya awali haijulikani vizuri. Japokuwa kinachojulikana ni kwamba mbwa wa Sheltie ni kutoka katika uzao wa Collie. Sheltie ni uzao wa mbegu ya mbwa jamii ya Scottish Collie na King Charles Spaniel. Iliendelezwa kwa nia ya kuchunga kondoo katika Kisiwa cha Shetland, ambako fukwe zake zenye miinuko zimesababisha kuwepo kwa wanyama wengine wadogo.

Lakini leo hii Sheltie ni mbwa wanafugwa kwa ajili ya ulinzi shambani na kama wanyama wa mapambo. Awali walikuwa wadogo sana wakiwa na kimo cha inchi 8 hadi 12 kutoka mabegani kabla ya kuwapandisha na jamii ya Collie kupata jamii ya sasa.

Kwa ujumla, mbwa wa jamii ya Sheltie wana uzito wa kilogram 5 hadi 11. Madume yana urefu wa sentimeta 37 na majike 36.

Sheltie wana uwezo mkubwa wa akili na wanashika nafasi ya sita kati ya jamii 132 za mbwa duniani.

Japokuwa ni wafupi, lakini wanaweza kuruka hata kwenye ukuta wa urefu wa meta moja na nusu na wanashiriki katika michezo mbalimbali ya mbwa.

7 - LABRADOR RETRIEVER

 Mbwa wa jamii ya Labrador Retriever, ambao pia wanafahamika tu kama Labrador, wako katika kundi la mbwa watafutaji na wachunguzi. Jamii hii ya mbwa ni miongoni mwa mbwa maarufu Marekani na Uingereza.

Kutokana na uwezo wao, Labrador wanafundishwa kuwaongoza wasioona katika nchi nyingi, lakini pia wanatumiwa na polisi katika sehemu mbalimbali kwa ajili ya kunusa vitu vya hatari zikiwemo dawa za kulevya na kadhalika.

Awali mbwa wa Labrador Retriever walifahamika kama St. John's water dog, mbwa wa St. John, au Lesser Newfoundland. Wakati mbwa hao walipopelekwa England katika eneo la Labrador ndipo wakaitwa Labrador Retrievers kwa sababu walitumika kuzamia na kutafuta vitu kwenye Bahari ya Labrador.

Mbwa wa Labrador wana maumbile ya kati na makubwa, huku madume yakiwa na uzito wa kati ya kilogram 29 na 36 na majike kilogram 25 na 32. Kimo chao ni kati ya sentimeta 57 na 62 kwa madume na sentimeta 55 na 60 kwa majike.

Mbwa hawa ni wakali wanapowajibika, lakini ni wapole kwa ujumla wake, wanapenda kutembea na wana asili ya kuchunguza sana, ndiyo maana ni rahisi kuwafundisha hata kutafuta vitu mbalimbali. Wanatumika kwenye majeshi ya majini na nchi kavu. Wanaweza kufuatilia na kuwachunguza wanamagendo.

Wana uwezo mkubwa wa kunusa na ndiyo maana hata polisi huwatumia kunusa harufu ya vvitu mbalimbali, ikiwemo dawa za kulevya, kutambua wanamagendo, wezi, magaidi na kadhalika.

Mbwa hawa wanaweza uwezo wa kuishi kati ya miaka 10 na 12.

8 – PAPILLON - KIPEPEO

Mbwa jamii ya Papillon ni wadogo kutoka jamii ya mbwa wanasesere wa Continental Toy Spaniel. Pamoja na udogo wao, lakini mbwa hawa ambao ni jamii ya zamani sana wana akili. Papillon ni jina la Kifaransa ambalo maana yake ni ‘kipepeo’ na Wafaransa, ambako ndiko iliko asili ya mbwa hao, walimwita hivyo kwa jinsi alivyo mdogo.

Mbwa hawa daima ni marafiki na wanapenda kutembea sana. Hawana aiba na wana nguvu. Japokuwa ni mbwa mwenye urafiki, lakini lazima kumwangalia anapokuwa na watoto, kama ilivyo kwa mbwa wengine, kwa sababu akichokozwa ni balaa.

Mbwa huyu, pamoja na udogo wake, lakini ana uwezo wa kuishi hadi miaka 17.

9 – ROTTWEILER

Rottweiler ni jamii ya mbwa mwenye umbile la kati na kubwa ambaye asili yake ni Ujerumani ambako walijulikana kamaRottweiler Metzgerhund, ambayo maana yake ni mbwa wachinjaji wa Rottweil, yaani Rottweilbutchers' dogs, kwa sababu mojawapo ya kazi zao ilikuwa kuchunga ng’ombe na mifugo mingine na kuvuta mikokoteni yenye nyama kwa ajili ya kupeleka sokoni.

Hii iliendelea hadi katikati ya karne ya 19 wakati wa ujio wa reli ambapo sasa kazi yao ikabakia kuchunga mifugo.

Kwa sasa mbwa hawa wanatumika kama watafutaji na waokoaji, mbwa waongozaji kwa wasioona, mbwa walinzi na mbwa wa polisi

Mbwa wa umbile la kawaida ana urefu wa sentimeta 61 hadi 69 kwa dume, wakati jike ni sentimeta 56 hadi 63, na wana uzito wa kilogram kati ya 50 na 60 kwa dume na kilogram 35 na 48 kwa jike.

Usicheze na mbwa hawa, kwa sababu licha ya utii, ukakamavu, welekevu na jitihada ya kazi, lakini ni wakali. Ukimwamuru tu, kazi imekwisha.

Kama mfugaji wa mbwa jamii ya Rottweiler hatakuwa makini, anaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii na ndiyo maana wengi wanafugwa hata na majeshi ambako wanaweza kuwadhibiti.

Mbwa hawa wanaweza kuishi kati ya miaka 8 hadi 10.

10 - AUSTRALIAN CATTLE DOG


Australian Cattle Dog (ACD), auCattle Dog, ni mbwa mchunga ng’ombe ambaye asili yake ni Australia ambako alifugwa maalum kwa kuchunga ng’ombe katika maeneo ambayo ni vigumu binadamu kupita kwa urahisi.

Mbwa hawa wana maumbile ya kati, wana nguvu, wakakamavu na wana akili huku wakipendelea zaidi kuwa huru, siyo kufuatwa fuatwa.

Wanaitikia vyema kwenye mafunzo, hasa kama mafunzo hayo yanavutia na magumu.

Awali walifugwa kwa ajili ya kuchunga kwa kuwang’ata ng’ombe. Ni mbwa walinzi wazuri kwa familia kwa sababu wanaweza kumwelewa kila mtu ndani ya familia, ambapo kama itatokea mwanafamilia yuko hatari, wanaweza kutokea kusaidia.

Mbwa hawa wanaweza kuishi kati ya miaka 12 hadi 14.

NI JUU YAKO, UNATAKA KUFUGA MBWA WA AINA GANI KATI YA HAWA.

Post a Comment

Previous Post Next Post