Jinsi ya Kumzoeza Mbwa Wako


“MBWA wangu haji ninapomwita.” “Mbwa wangu hubweka sana hivi kwamba majirani wanalalamika.” “Kila mara mbwa wangu hunirukia na kuwarukia wageni wangu.” Katika visa vyote hivyo, watu wanaofuga wanyama-vipenzi wanauliza, “Nifanye nini?”

Huenda ukahitaji kumfundisha mbwa wako kutii mambo ya msingi, yaani, kumfundisha kutii amri rahisi. Bila shaka, inafaa kuanza kumfundisha akiwa mdogo. Lakini hata mbwa wazee wanaweza kujifunza. Marcos, mtaalamu wa kuzoeza mbwa nchini Mexico, anasema: “Mbwa wachanga zaidi tunaozoeza wana umri wa miezi minne na wale wazee zaidi wana umri wa miaka mitano. Lakini, hata nimewafundisha mbwa wenye umri wa miaka kumi kutii mambo ya msingi.”

Mbwa ni werevu. Wamezoezwa kunusa dawa za kulevya na vitu vinavyoweza kulipuka, kuwasaidia walemavu, na pia kuwatafuta na kuwaokoa watu walio hatarini. Lakini unawezaje kumzoeza mbwa wako akutii?

Tabia za Mbwa

Kwanza unahitaji kujua tabia za mbwa wako. Sawa na mbwa-mwitu, katika jamii ya mbwa kuna vyeo mbalimbali. Kiasili, wao hupendelea kuishi wakiwa kikundi kilicho na kiongozi. Mbwa wako huiona familia yako kuwa kikundi chake, na anapaswa kutambua kwamba wewe ndiwe kiongozi.

Kiongozi katika kikundi cha mbwa-mwitu hulala mahali penye joto zaidi na palipoinuka zaidi. Pia yeye hula kabla ya wengine. Hivyo, ukimruhusu mbwa wako alale juu ya kitanda chako au juu ya viti, huenda akajiona kuwa kiongozi. Atahisi hivyo pia akipewa chakula kutoka mezani wakati mnapokula.

Hata akiwa mchanga, mbwa wako anaweza kujifunza kwamba wewe ndiwe kiongozi. Jinsi gani? Jaribu kumkazia macho kwa muda mrefu hadi aache kukutazama. Pia, itafaa umpapase-papase tumboni huku akiwa ameulalia mgongo wake kwa sababu hilo humfanya ajitiishe. Mbwa wako akikusumbua na kuendelea kufanya hivyo hata unapomwamuru aache, jaribu kumpuuza au kuondoka.

Mbwa wako anapokutii, anaonyesha kwamba anakutambua kuwa kiongozi. Usipomwonyesha mbwa wako kwamba wewe ndiwe kiongozi, huenda akafikiri kwamba mna cheo sawa naye au yeye ndiye mkubwa wako, na hilo linaweza kuathiri tabia yake.


Jinsi ya Kumfundisha Amri Rahisi

Ili kumfundisha mbwa wako amri rahisi utahitaji mshipi wa shingoni, mkanda, na kuwa mwenye subira nyingi. Kitabu kimoja chenye maagizo ya kuzoeza mbwa kinapendekeza hivi: (1) Toa amri fupi na rahisi, (2) mwonyeshe unachotaka afanye, na (3) msifu mara tu baada ya kutii. Jinsi unavyotoa amri ni muhimu zaidi ya maneno unayotumia. Amri inapaswa kutolewa kwa sauti yenye mkazo, nayo pongezi inapaswa kutolewa kwa furaha na uchangamfu.

Si lazima kumpiga mbwa unapotoa nidhamu. Marcos, yule mtaalamu wa kuzoeza mbwa aliyetajwa mapema, anasema: “Mimi husema tu kwa mkazo ‘Wacha’ ili mbwa ajue kwamba sifurahii anachofanya.” Anaongeza hivi: “Mbwa ni mwerevu na anajua unapompongeza na unapomkemea.”

Ukihitaji kuchukua hatua zaidi, unaweza kumshika mbwa nyuma ya shingo na kumtikisa polepole huku ukisema “Wacha.” Kemeo linapaswa kutolewa mbwa anapokosea au mara tu baada ya hapo. Kumbuka kwamba mbwa hawezi kuelewa sababu ya kukemewa ikiwa anakemewa muda mrefu baada ya kukosea. Pia hataweza kuelewa kwa nini tendo fulani linafaa wakati mmoja lakini halifai anapolifanya wakati mwingine. Kwa hiyo, usiwe kigeugeu.

Amri ya msingi ni “Keti!” Mbwa wako akijua amri hii, unaweza kumdhibiti anaposisimuka sana. Kwa mfano, unaweza kumwambia mbwa wako aketi anapowarukia wageni. Ili kumfundisha mbwa wako kuketi, mfunge kwa mkanda na umwamuru aketi huku ukimsukuma sehemu zake za nyuma na kuvuta kichwa chake taratibu kwa mkanda. Mpongeze papo hapo. Rudia kufanya hivyo mpaka mbwa anapoweza kutii amri hiyo bila msaada.

Ili kumfundisha mbwa wako kuendelea kuketi, simama mbele yake na unyooshe mkono wako kumwelekea huku ukimwambia “Kaa hapo!” Mbwa akisonga, mwambie “Wacha” na umrudishe mahali alipokuwa. Rudia amri hiyo, na umsifu mbwa akiendelea kuketi kwa muda mfupi. Anapotii, mwache aketi kwa muda mrefu zaidi hatua kwa hatua na uongeze umbali kati yako naye.

Njia bora ya kumfundisha mbwa wako kuja mahali ulipo ni kutumia mkanda mrefu na kumvuta kidogo, huku ukimwita kwa jina na kumwambia “Njoo!” Songa nyuma mbwa anapozidi kukukaribia na uendelee kumpongeza. Baada ya muda atatii amri yako bila kuhitaji kuvutwa kwa mkanda. Mkanda wa mbwa wako ukitoka, naye akatae kuja unapomwambia “Njoo!” mwite na ukimbie upande ule mwingine. Mara nyingi mbwa atakufuata mbio.

Tahadhari: Usitumie neno “njoo” wakati usiofaa, kama vile unapotaka kumkemea mbwa. Mbwa wako anapaswa kujifunza kwamba atafaidika unapomwambia “Njoo,” labda kwa kusifiwa au kupewa chakula. Ukikosa subira unapomfundisha amri hiyo, mbwa wako atajifunza kwamba kuja wakati unapomwita si jambo zuri na linapaswa kuepukwa.

Pia unaweza kumfundisha mbwa wako kutembea kando yako bila kuwa mbele yako au kubaki nyuma yako. Ili kufanya hivyo, tumia mshipi wa shingoni uliounganishwa na mkanda mfupi. Mbwa wako akiwa upande wa kushoto, mwambie “Tembea!” kisha uanze kutembea kwa mguu wako wa kushoto. Mbwa wako akijaribu kwenda mbele yako au kubaki nyuma, vuta mkanda haraka na kwa nguvu huku ukirudia amri hiyo. Mpongeze anapotii.

Unawezaje kumzuia mbwa wako asikurukie? Njia moja ni kusonga nyuma huku ukimwambia “Toka!” kisha umwambie “Keti!” Njia nyingine ni kushika miguu yake ya mbele kwa mikono yote miwili na kumkaribia huku ukimwambia “Toka!” tena na tena. Mpongeze anapotii.

Rafiki Mwaminifu

Kumbuka kwamba mbwa ni mwenye urafiki. Kutengwa au kufungiwa sana kunaweza kumfanya awe msumbufu, abweke kupita kiasi, na kuharibu vitu. Mbwa wako akizoezwa, anaweza kuwa rafiki mwaminifu mwenye kupendeza badala ya kuwa msumbufu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

Madokezo ya Kumzoeza Mbwa

1. Usibadili maneno unayotumia kutoa amri.

2. Mbwa hupenda kusikia jina lake, naye huitikia linapotumiwa. Hivyo, tumia jina la mbwa wako unapotoa amri. (“Popi, keti!”) Lakini usitumie jina lake unapomkemea, kama vile kumwamuru “Wacha!” Mbwa wako anapaswa kujifunza kwamba atafaidika wakati unapomwita kwa jina wala hutamkemea.

3. Mpongeze mbwa wako mara nyingi. Mbwa wengi hufurahia kupongezwa zaidi ya kupewa chakula.

4. Mzoeze kwa vipindi vifupi na vinavyofurahisha.

5. Usimfundishe mbwa wako tabia mbaya bila kujua kwa kumkazia fikira sana anapokosea. Hilo litamfanya arudie tabia hiyo mbaya.

[Picha]

Mpongeze

“Popi, keti!”

[Hisani]

Yametolewa katika kitabu Never, Never Hit Your Dog na American Dog Trainers Network.

Kumfundisha Mbwa Wako Mdogo Kwenda Haja Nje

Mbwa anaweza kufundishwa kwenda haja nje ya nyumba anapokuwa na umri wa majuma sita hadi nane. Kulingana na kitabuDog Training Basics, njia yenye mafanikio zaidi ya kumfundisha mbwa kwenda haja nje ni kumfungia, kumzoeza, kumwekea wakati wa kwenda haja, na kumpongeza. Kwa kawaida mbwa hapendi kwenda haja mahali anapolala. Hivyo, mfungie mbwa mdogo wakati ambapo hakuna mtu wa kumtunza. Chunguza wakati hususa ambapo yeye huenda haja, na umtengee mahali pamoja pa kufanya hivyo. Mpeleke hapo (kwa mkanda) mara tu anapoamka, anapomaliza kula, baada ya kucheza, au kabla ya kulala. Mpongeze anapomaliza haja. Unaweza kumfundisha neno linaloonyesha wakati unaofaa na mahali panapofaa kwenda haja.

Wakati ambapo mbwa wako mdogo hajafungiwa, uwe chonjo kutambua dalili zinazoonyesha kwamba anataka kwenda haja, kama vile kuacha kucheza ghafula, kuzunguka-zunguka huku akinusa-nusa, na kukimbia nje ya chumba. Ukimpata mbwa wako mdogo akienda haja ndani ya nyumba, mkemee na umpeleke nje mara moja.*Kumbuka, hutamfundisha lolote kwa kumkemea muda mrefu baada ya kukosea. Safisha uchafu kwa maji ya siki ili kuondoa uvundo, la sivyo, mbwa ataendelea kwenda haja hapo.

[Maelezo ya Chini]

Ni kawaida mbwa kukojoa anapokusalimu kwa uchangamfu. Nyakati nyingine huo huitwa mkojo wa kujitiisha, na unaweza kumaanisha kwamba anakutambua kuwa kiongozi. Kumkemea mbwa wako wakati huo hakutasaidia, kwani kutamfanya tu akojoe zaidi ili kuonyesha kwamba anakutambua kuwa mwenye mamlaka. Kwa kawaida, mbwa anapofikia umri wa miaka miwili, yeye huacha tabia hiyo.

2 Comments

Post a Comment

Previous Post Next Post