Kutunza kumbukumbu za shamba la samaki na masoko

Kumbukumbu ambazo ni muhimu kwa ajili ya kutunzwa ni kama, ukubwa wa bwawa, idadi ya samaki, sehemu mbegu ilipochukuliwa, uzito wa mwanzo wa samaki, tarehe ya kupanda samaki, kiwango cha chakula kwa kila siku/wiki/mwezi, ubora wa maji, mahitaji ya kila siku na gharama zake , tarehe ya kuchukua sampuli, na wastani wa uzito wa samaki kwa kila mwezi.

Taarifa hizi ni muhimu sana kwa ajili ya kufanya tathmini ya mradi, hivyo itakusaidia kujua kama mradi wako unakupatia faida au hasara.

Faida za kutunza kumbukumbu

Utunzaji wa kumbukumbu sahihi utasaidia mambo yafuatayo;

Kufuatilia shughuli zote shambani na kutathmini gharama zote za usimamizi na uendeshaji wa shughuli za shambani.

Zinasaidia kuboresha utendaji wa shughuli shambani na kuweza kupata historia ya mradi.

Changamoto zinazoathiri ufugaji wa samaki

• Ukosefu wa mbegu bora na za kutosha.

• Kukosekana kwa wataalamu wa kutosha katika kutoa huduma za ugani hasa vijijini. Pia wataalamu wachache waliopo bado hawajawezeshwa vizuri ili wawafikie wakulima.

• Kukosekana kwa masoko ya uhakika (hasa kwa upande wa kambale).

• Kukosekana kwa tafiti za kutosha juu ya ufugaji wa samaki katika maeneo yetu. Pia hakuna muunganiko mzuri kati ya watafiti wachache waliopo na wafugaji samaki. Hivyo matokeo ya tafiti chache zilizofanywa haziwafikii wafugaji moja kwa moja.

• Kukosekana kwa wataalamu wa kutosha katika upande wa vinasaba (genetics) na magonjwa ya samaki.

• Kukosekana kwa sera bora ya ufugaji samaki.

• Mlolongo mrefu katika kupata vibali vya ufugaji samaki (kwa wanaotaka kufanya miradi

mikubwa ya ufugaji samaki).

• Ukosefu au uhaba wa mitaji kwa wafugaji walio wengi.

Magonjwa

Ufugaji wa samaki huusisha kutoa mbegu sehemu moja hadi nyingine hivyo kama hakutakuwa na umakini wa kutosha basi magonjwa yanaweza kuenezwa katika maji ya asili. Kwa maana hiyo, ni muhimu samaki wageni kabla ya kuwaweka bwawani, watengewe eneo maalumu kwa ajili ya kuchunguza kama kuna magonjwa au visababishi vya magonjwa.

Maji machafu

Kwa kawaida ufugaji unahitaji kubadilisha maji na pia hata kutoa maji yote bwawani wakati wa kuvuna samaki. Kwa maana hiyo, kama maji yataachiwa moja kwa moja kwenda kwenye mazingira au kwenda kwenye maji ya asili yatasababisha uharibifu. Kabla ya maji kuachiwa ni lazima yatibiwe au kuchujwa kwa utaratibu unaotakiwa. Pia ni vizuri zaidi kama maji toka mabwawani yatatumika kwa kilimo cha mazao na hasa mbogamboga na matunda.

Ukataji wa miti/mikoko

Ufugaji wa kambale umekuwa ukihusisha ukataji wa mamia ya hekari za mikoko ambazo hutumiwa na samaki kama sehemu za kuzalia, kula na kujificha. Pia mikoko husaidia kuzuia mmomonyoko wa kingo za bahari na hata kuzuia majanga kwa binadamu kama sunami.

Hivyo ni vizuri wakati wa kuchagua eneo la kufugia samaki kuzingatia na kuzuia uharibufu wa mazingira ili kuweza kupata mahitaji ya sasa nay a baadaye kwa kuhifadhi mikoko na miti mingine pia.

Utumiaji wa madawa/kemikali

Katika ufugaji wa samaki, magonjwa yanaweza kutokea kama kanuni za ufugaji hazijazingatiwa. Hivyo  basi, madawa yatatumika ili kuokoa samaki na ni vizuri madawa yasitumiwe kiholela kwani husababisha madhara kwa viumbe wengine na hata binadamu.

Kutoroka kwa samaki wageni

Samaki wageni wanaweza kutoroka kupitia maji machafu na kuruka na kuingia kwenye maji ya asili na hasa katika mfumo wa cage. Samaki wanaotoroka wanaweza kusababisha samaki wa asili kutoweka endapo waliotoroka watawala wale wa asili au wakasababisha mchanganyiko wa vinasaba hivyo kuathiri kizazi cha awali.

Soko

Soko ni jambo la muhimu sana kujua kabla ya kuanzisha mradi wa ufugaji wa samaki. Kabla ya kuanzisha mradi, mfugaji ni lazima ajiulize maswali haya; Je, nitauza wapi samaki wangu baada ya kuvuna? Je, ni kwa kiasi gani na wakiwa katika hali gani? Je, ni mara ngapi (kila siku/wiki/mwezi au mwaka) na nitawauza kwa shilingi ngapi? Taarifa hizi ni muhimu kwani zitakusaidia kujua ufanye mradi wa ukubwa gani na utumie mfumo upi wa ufugaji?

Pia ni vizuri kujua mfumo utakaotumika kuuza samaki wako, mfano; ukiuza samaki wengi kwa wakati mmoja utauza kwa bei ya jumla ambayo ni ndogo ukilinganisha na kuuza kwa rejareja. Kwa maana hiyo, mfumo wa kuuza samaki wako utategemeana na ukubwa wa mradi.

Kama mradi ni mkubwa, itakuwa ni vigumu kuuza kidogokidogo lakini kama mradi ni mdogo uza samaki wako rejareja ili upate faida nzuri. Chunguza wateja wako wanataka samaki awe katika hali gani sokoni; kama samaki hai, waliogandishwa, waliokaangwa, waliowekewa chumvi na waliokaushwa kwa moshin au jua.

Vitu muhimu wa kuzingatia katika masoko ya samaki

Uhakika wa bidhaa

Hakikisha unaweza kuhudumia soko au wateja kwa wakati unaofaa, kama mteja anahitaji samaki kila wiki mara moja basi panga mpango mzuri shambani kwako. Kwa mfano; unaweza kuwa na mabwawa kadhaa ambayo utapanda samaki kwa muda tofautitofauti ili uweze kupata idadi ya samaki wanaohitajika katika uzito unaotakiwa.

Ubora wa samaki

Ukubwa, mwonekano na ladha ni muhimu vikazingatiwa pindi samaki wawapo bwawani hadi kuvuna. Wakati wa kuvuna hakikisha samaki wako hawapati majeraha na pia hawatumii nguvu nyingi ili wasiharibike mapema. Samaki baada ya kuvuliwa wahifadhiwe vizuri kwa ajili ya kuhakikisha ubora mzuri.

Matangazo

Ni vizuri kujitangaza kwa kutumia njia mbalimbali kama vile magazeti, televisheni, radio na hata mitandao ya kijamii. Pia utaweza kuwasiliana na wamiliki wa hoteli, migahawa, mashulena taasisi nyingine ambazo wanatoa huduma ya chakula kwa watu wao.

Hali ya samaki katika vyanzo vya asili

Kabla ya kuvuna samaki chunguza hali ya uvuvi katika maji ya asilia yaani mito, maziwa na bahari. Uvuvi katika maeneo haya haufananii katika majirayote ya mwaka, hivyo ni vizuri kujua msimu ambao uvuvi katika maji asilia hupungua.

Pindi uvivu wa samaki unapokuwa chini hufanya hitaji la samaki kuwa juu katika soko na kupelekea samaki kuuzwa kwa bei kubwa. Kwa mfano, upepo mkali huadhiri kazi za uvuvi hivyo basi siku zenye upepo mkali zinaweza kuwa siku nzuri za kuvuna na kupeleka samaki wako sokoni. 

Post a Comment

Previous Post Next Post